Matokeo Ya Kuhesabiwa Haki
 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2
                                ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii
                                ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu
                                la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5
                                wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina
                                pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.
6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.
 9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10
                                Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya
                                kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa
                                uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.
Adamu Alileta Kifo, Yesu Ameleta Uzima
 12
                                Kwa hiyo kama vile dhambi ilivyoingia ulimwenguni kupitia kwa mtu
                                mmoja, na kupitia dhambi hii mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote
                                wamefanya dhambi: 13 kwa maana kabla sheria haijatolewa, dhambi ilikuwepo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi wakati hakuna sheria. 14
                                Hata hivyo, tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Mose, mauti ilitawala
                                watu wote, hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa kuvunja amri, kama
                                alivyofanya Adamu, ambaye alikuwa mfano wa yule atakayekuja.
 15
                                Lakini ile karama iliyotolewa haikuwa kama lile kosa. Kwa maana ikiwa
                                watu wengi walikufa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja, zaidi sana neema ya
                                Mungu na ile karama iliyokuja kwa neema ya mtu mmoja, yaani, Yesu
                                Kristo, imezidi kuwa nyingi kwa ajili ya wengi. 16Tena,
                                ile karama ya Mungu si kama matokeo ya ile dhambi. Hukumu ilikuja kwa
                                njia ya mtu mmoja, ikaleta adhabu, bali karama ya neema ya Mungu ilikuja
                                kwa njia ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. 17Kwa
                                maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo
                                mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama
                                yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mtu
                                mmoja, yaani, Yesu Kristo.
 18
                                Kwa hiyo, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta adhabu kwa watu wote,
                                vivyo hivyo pia kwa tendo la haki la mtu mmoja lilileta kuhesabiwa haki
                                ambako huleta uzima kwa wote. 19
                                Kwa maana kama vile kwa kutokutii kwa yule mtu mmoja wengi walifanywa
                                wenye dhambi, vivyo hivyo kwa kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye
                                haki.
 20 Zaidi ya hayo, sheria ilikuja, ili uvunjaji wa sheria uongezeke. Lakini dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi, 21
                                ili kwamba kama vile dhambi ilivyotawala kwa njia ya mauti, vivyo hivyo
                                neema iweze kutawala kwa njia ya kuhesabiwa haki hata kuleta uzima wa
                                milele katika Yesu Kristo Bwana wetu.
JIBU MASWALI.
										
			