WARUMI5

Matokeo Ya Kuhesabiwa Haki

1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2
ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii
ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu
la kushiriki utukufu wa Mungu.
3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5
wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina
pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10
Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya
kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa
uzima wake.
11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

Adamu Alileta Kifo, Yesu Ameleta Uzima

12
Kwa hiyo kama vile dhambi ilivyoingia ulimwenguni kupitia kwa mtu
mmoja, na kupitia dhambi hii mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote
wamefanya dhambi:
13 kwa maana kabla sheria haijatolewa, dhambi ilikuwepo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi wakati hakuna sheria. 14
Hata hivyo, tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Mose, mauti ilitawala
watu wote, hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa kuvunja amri, kama
alivyofanya Adamu, ambaye alikuwa mfano wa yule atakayekuja.

15
Lakini ile karama iliyotolewa haikuwa kama lile kosa. Kwa maana ikiwa
watu wengi walikufa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja, zaidi sana neema ya
Mungu na ile karama iliyokuja kwa neema ya mtu mmoja, yaani, Yesu
Kristo, imezidi kuwa nyingi kwa ajili ya wengi.
16Tena,
ile karama ya Mungu si kama matokeo ya ile dhambi. Hukumu ilikuja kwa
njia ya mtu mmoja, ikaleta adhabu, bali karama ya neema ya Mungu ilikuja
kwa njia ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki.
17Kwa
maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo
mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama
yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mtu
mmoja, yaani, Yesu Kristo.

18
Kwa hiyo, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta adhabu kwa watu wote,
vivyo hivyo pia kwa tendo la haki la mtu mmoja lilileta kuhesabiwa haki
ambako huleta uzima kwa wote.
19
Kwa maana kama vile kwa kutokutii kwa yule mtu mmoja wengi walifanywa
wenye dhambi, vivyo hivyo kwa kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye
haki.

20 Zaidi ya hayo, sheria ilikuja, ili uvunjaji wa sheria uongezeke. Lakini dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi, 21
ili kwamba kama vile dhambi ilivyotawala kwa njia ya mauti, vivyo hivyo
neema iweze kutawala kwa njia ya kuhesabiwa haki hata kuleta uzima wa
milele katika Yesu Kristo Bwana wetu.

JIBU MASWALI.

 QUIZ