Abrahamu Alihesabiwa Haki Kwa Imani
1 Tuseme nini basi, kuhusu Abrahamu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili? 2 Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu. 3 Kwa maana Maandiko yasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”
4 Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili. 5 Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki. 6 Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena juu ya baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo:
7 “Wamebarikiwa wale
ambao wamesamehewa makosa yao,
ambao dhambi zao zimefunikwa.
8 Heri mtu yule
Bwana hamhesabii dhambi zake.”
Haki Kabla Ya Tohara
 9
                                Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa
                                wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa
                                haki.” 10
                                Je, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au
                                baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa. 11
                                Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani
                                hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote
                                wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki. 12
                                Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa
                                tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Abrahamu alikuwa
                                nayo kabla ya kutahiriwa.
Ahadi Ya Mungu Hufahamika Kwa Imani
 13
                                Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au
                                kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa
                                imani. 14 Kwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, 15 kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa.
 16
                                Kwa hiyo, ahadi huja kwa njia ya imani, ili iwe ni kwa neema, na
                                itolewe kwa wazao wa Abrahamu, si kwa wale walio wa sheria peke yao,
                                bali pia kwa wale walio wa imani ya Abrahamu. Yeye ndiye baba yetu sisi
                                sote. 17
                                Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye
                                ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anaye
                                fufua waliokufa, na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba
                                vimekwisha kuwako.
Mfano Wa Imani Ya Abrahamu
 18
                                Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akawa baba wa
                                mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Uzao wako utakuwa mwingi
                                mno.” 19
                                Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri juu ya mwili wake,
                                ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka
                                mia moja, au alipofikiri juu ya ufu wa tumbo la Sara. 20 Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, 21 akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi. 22 Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.” 23 Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake, 24 bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupa haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu. 25 Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.
JIBU MASWALI.
										
			